Skip to content
March 29, 2016 / bswitaba

Je, Tanzania ni mfano mwema Kidemokrasia Barani Afrika?

Rais Mteule wa Zanzibar
Picha: Rais Mteule wa Zanzibar Ali Mohamed Shein
Hisani: Daily News

Mwezi Oktoba mwaka jana, Tanzania iliandaa uchaguzi mkuu na mgombea wa CCM Mhe. John Pombe Magufuli akatangazwa na NEC kama mshindi, na kuwa rais wa tano wa jamhuri ya muungano.
Ila kisiwani Zanzibar, matokeo ya urais yalifutiliwa mbali na tume ya uchaguzi ZEC. Hali hii ilipelekea Upinzani CUF kuzua pingamizi. Ni bayana kuwa upinzani ulikuwa umetwaa ushindi lakini tume ya uchaguzi kisiwani ZEC iliamua kubatilisha matokeo kwa kigezo kuwa yalikuwa yamekumbwa na udanganyifu . Wadadisi wa maswala ya kisiasa waliona hatua hii ya ZEC kama njama ya kujaribu kukinusuru chama tawala kupitia marudio ya uchaguzi.
ZEC ilitangaza kuwa shughuli nzima ya uchaguzi ingerejelewa upya kisiwani Zanzibar .
Licha ya kuandaa mikakati ya uchaguzi mpya kisiwani humo wiki hii, upinzani uliamua kususia harakati hizo kwayo kumwacha mgombea wa chama tawala cha CCM Ali Mohamed kujimwaya ulingoni bila mshindani, na kuweza kutamba safari hii na asilimia tisini (90%) ya kura.

Nchi za magharibi zimekuwa zikiisifia Tanzania kwa kuwa mfano mwema katika demokrasia barani Afrika. Kwa jumla, imelinganishwa na nchi kama vile Ghana na Botswana.
Ni bayana kwamba wakati nchi jirani zimekuwa zikipitia vipindi na hali tatanishi za msukosuko kisiasa, Tanzania imeweza kuimarisha mabadiliko kisiasa bila ya kushuhudia hali ya mtafaruku katika kipindi cha miaka 55 ya uhuru wake.

Mtazamo wa Hali Halisi ya Demokrasia Nchini Tanzania

Je, demokrasia nchini Tanzania ni ya mfano mwema kama inavyodaiwa na nchi za magharibi au ni ya kutamausha tu?
Ili kupata jibu mwafaka kwa hili swala, itabidi tujiulize ni nini haswa kinachangia demokrasia halisi?
Kwa kawaida, demokrasia iliyonawiri inazingatia kanuni na misingi iliyowekwa ya demokrasia kama vile uzingatiaji wa sheria, kuheshimu maoni au misimamo ya kisiasa inayotofautiana, ujumuishwaji wa upinzani na mashirika ya umma kwenye maswala yenye umuhimu katika taifa mfano utengenezaji wa katiba, uwajibikaji kwa wananchi, na vile vile uhakikishaji wa mazingira yanayowezesha uchaguzi ambao ni  huru, wa haki na ukweli.
Ili kupima kama kweli Tanzania imekaribia kutimiza haya yote, hebu tuchambue jinsi hali ilivyo:

Kuondoka kwa Rais Kikwete usukani na kumkabidhi ala za uongozi Rais Magufuli ni ishara dhati kuwa Tanzania inazingatia kanuni zilizowekwa kuhusu mihula ya urais.
Hapa Tanzania inajizolea alama tele, ukizingatia kuwa marais wengine barani Afrika wamefutilia mbali swala la mihula na hata kujitanganza marais milele.
Tanzania inastahili pongezi kwa kuwa na vipindi vya mpwito kutoka kwa rais mmoja hadi mwingine.
Wasifu huu mzuri ulifanikishwa na baba mwanzilishi wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye aliamua kung’atuka mamlakani mnamo mwaka wa 1985 japo kipindi kile hakukuwepo na swala la kizingiti katika mihula. Kwa kweli sio kawaida kwa marais wa Afrika kung’atuka mamlakani. Kando na Mwalimu Nyerere, rais mwingine aliyeng’atuka mamlakani japo bado alikuwa  na muhula mwingine wa kuhudumu ni Mandela wa Afrika Kusini.

Licha ya hayo, kwenye maswala ya uzingatiaji wa sheria, kuheshimu maoni au misimamo ya kisiasa inayotofautiana, ujumuishwaji wa upinzani na mashirika ya umma kwenye maswala yenye umuhimu katika taifa, Tanzania imefeli kabisa.
Ukizingatia utengenezaji wa katiba rasimu, chama tawala kilidhihirisha ubabe kwa kiendesha shughuli hii bila ya kuwashirikisha wadau muhimu. Wengi walibaki kukisuta chama tawala na hata kukilinganisha na siha ya dalali.
Wakereketo wa CMM hawakukosa cheche za majibu kwa kudai upinzani ni kama chinga anayeuza chochote ili mradi amshawishi mpiga kura

Utawanyaji wa mikutano ya upinzani wakati wa kampeni na jeshi la polisi sio jambo jipya.
Kuzidisha, kitengo cha vijana cha CCM kinajulikana sana kwa kushambulia ngome za upinzani pamoja na wafuasi wao haswa kwenye yale maeneo yanayo onekana kana kwamba yanaegemea upinzani. Mfano mufti ni maeneo ya Arusha na Zanzibar kisiwani ambayo yameweza kushuhudia hali ya ghasia wakati wa uchaguzi, wafuasi wa upinzani wakiwa walengwa wakuu.

Mashirika ya kijamii nayo yameishia kubanwa yasiwe na sauti au uhuru wa kusema, kinyume na ilivyo kwenye demokrasia halisi.
Chama tawala daima kinaunda sheria zinazikandamiza mashirika haya pamoja na vyombo vya habari.
Vile vile, swala la uwazi na uwajibikaji wa serikali kwa wananchi limesalia kuwa ndoto tu. Jambo lingine linalojitokeza ni lile la watu wenye nyadhifa kubwa serikalini kujihusisha kwenye sakata na ufisadi pasipo na kujali. Washukiwa wakuu kwenye sakata ya Escrow bado hawajachukuliwa hatua za kisheria hadi wa leo.
Sakata hii ya mwaka wa 2014 ilishuhudia kupotea kwa mamilioni ya dollar za Marekani zinazokadriwa kuwa zaidi ya milioni 400.
Mamilioni haya yalihamishwa kutoka Benki kuu ya Tanzania na kugawanywa kinyume na sheria miongoni mwa viongozi wakuu serikalini.
Japo upinzani ulizua tetesi kuhusu sakata hii kubwa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Tanzania, upande wa serikali uliifumbia macho hadi pale mashirika ya ufadhili yalipoamua kukatisha ufadhili wa zaidi ya dollar milioni 558.

Hatimaye kila kunapoandaliwa uchaguzi nchini Tanzania, swala kuu husalia kuwa iwapo uchaguzi huo utakuwa huru, wa haki na ukweli. Tume ya uchaguzi NEC siku zote inasalia kuwa kitengo chenye umuhimu zaidi kinachowezesha CCM kukandamiza upinzani.
Mshirika huyu mkuu wa CCM anakihakikishia chama tawala kupata idadi kubwa ya wajumbe bungeni kwa kutumia mbinu za shauku kihisabati, hali inayoishia kuipa CCM mgao wa viti vingi na uwakilishi kwenye bunge.
Kwenye upande wao, CCM inatumia mbinu zote kisheria na hata zile zinazokiuka sheria kuhakikisha uhangaishwaji wa wale wasiokubaliana na maoni ya serikali.

Uchambuzi wa Mwisho

Nchi za Magharibi zinatoa mtazamo uliopinda kuhusu nchi ya Tanzania. Huenda wana sababu zao za kuwa na mtazamo huu kwa manufaa yao wenyewe ambayo wanayafahamu.
Labda wanahitaji kukumbushwa kusoma kitabu cha mcheshi Penelope Dyan chenye maudhui “If You Put Lipstick on a Pig-You Will Have A Beautiful Pig”.
Katika chapisho lao “Democratization in Africa: Progress and Retreat” (Tanzania’s missing Opposition), Barak Hoffman, na Lindsay Robinson wanasisitiza “Tanzania leo sio demokrasia, bali ni himaya iliyopo chini ya chama kimoja cha CCM”.
Iwapo baba mwanzilishi wa taifa Mwalimu Nyerere angeweza kurejea leo – je, angekuwa na lolote la kujivunia kidemokrasia nchini Tanzania au angesalia kutamaushwa na jinsi mambo yalivyo?  Haya msomaji kazi kwako, wewe yatafakari hayo.

Kuhusu Mwandishi
Bonface Witaba
:
Mwana teknohama wa tajriba ya juu nchini Kenya na mchanganuzi wa maswala ya utawala wa mitandao (Internet Governance), utafiti wa sera (Policy Research)
Pia ni Mshirika wa ICANN (ICANN Fellow-Singapore/Dublin), AFRINIC Fellow(Congo), CPRSouth Fellow-Yuan Ze University (Taiwan), na DiploFoundation (Switzerland).
Ameshirika kongamano nchi mbali mbali kutoa hisia zake, moja wapo likiwemo lile la utawala wa mitandaoni lililoandaliwa Brazil 2015 na umoja wa mataifa (UN Internet Governance Forum).

Maoni yaliyotolewa hapa ni yake binafsi na wala pasiwe na mwonekano kuwa yale ya mashirika anayohusiana nayo.

Kuwasiliana naye:

Twitter: @bswitaba

Advertisements

One Comment

Leave a Comment
  1. lyla / Mar 29 2016 3:43 pm

    Watanzania wanatakiwa kudai hatua kwa wezi wa Escrow. Bado demokrasia Yao haijakaa vzr.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: